News
Ubunifu wa Bidhaa za Wajasiriamali Tanzania wavutia wengi Maonesho ya Jua kali
Bidhaa za Wajasiriamali wa Tanzania katika maonesho ya 25 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi au Jua Kali zimekuwa kivutio kwa watu mbalimbali waliotembelea Banda la Tanzania kwenye Viwanja vya Uhuru Garden, Nairobi Kenya.
Wakizungumza Wajasiriamali hao kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania wamesema maonesho hayo ya 25 ya Nguvu Kazi au Jua Kali yamewapatia fursa ya kutangaza bidhaa zao, kubadilishana taarifa, kukuza ujuzi pamoja na masoko ya bidhaa na huduma.
"Bidhaa zetu wajasiriamali wa Tanzania zimekuwa kivutio sana katika haya maonesho kutokana na kutengeneza bidhaa zenye ubora na zilizothibitishwa," amesema Paul Onesmo
Kwa upande mwengine, Wajasiriamali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameonyesha kuvutiwa na bidhaa za wajasiriamali wa Tanzania na kueleza kuwa bidhaa hizo zina ubora wa hali ya juu.
"Nimetembelea banda la Tanzania na nineona wamekuja na bidhaa za kuvutia sana, ukiangalia ubunifu wa mavazi, viatu vya ngozi na vinyago kwa kweli ni nzuri sana," amesema Ndayiheke Nana-Myrna
Maonesho ya 25 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yanaongozwa na Kaulimbiu isemayo “Miaka 25 ya Ujumuishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki:Kuendeleza Ubunifu na Minyororo ya Thamani ya Kikanda kwa Biashara ndogo na za Kati Shindani kuelekea Maendeleo Endelevu”.
