Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Vijana kundi muhimu katika kukuza Uchumi wa Taifa - Waziri Ndalichako


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa Vijana ni kundi muhimu sana katika jamii na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Ameyasema hayo leo Februari 11, 2022 wakati wa ufunguzi wa Kongamano la vijana wa Kikristo na Ibada ya Kitaifa ya Maombi iliyofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, Jijini Dodoma.

Waziri Ndalichako alieleza kuwa, Vijana ni kundi muhimu ambapo kama taifa tunapaswa kulitumia vizuri ili kuweza kuleta maendeleo na kuliwezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kukuza uchumi wa Nchi.


“Serikali inatambua mchango wa vijana kwa Taifa lao, hivyo itaendelea kuhakikisha inawajenga vijana hapa nchini katika Nyanja zote ikiwemo za Elimu, Sayansi, Teknolojia, Ubunifu, Uchumi, Sanaa, Utamaduni na Michezo na mambo mengine mengi yanayolenga katika kuinua ustawi wa vijana,” alisema Waziri Ndalichako

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa takwimu vijana ni asilimia 35% ya idadi ya watu wote na pia ni kundi kati ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi, hivyo ni kundi muhimu sana linalotegemewa katika jamii na kukuza uchumi wa taifa.

Katika hatu nyingine Waziri Ndalichako amewafahamisha vijana kuwa, Serikali imeendelea kukuza na kusimamia masuala ya utoaji huduma za ajira nchini ili kuhakikisha fursa za ajira zinaongezeka kwa makundi yote hususan vijana na pia kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumu.



“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa nje na ndani kuwekeza nchini ambapo fursa hiyo imechangia vijana kujishughulisha kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ya kimkakati ikiwa ni pamoja na Mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, Mradi wa Treni ya Mwendo Kasi (SGR) na miradi mingine mingi ya Ujenzi ya inayoendelea kutekelezwa na Serikali,” alisema Mhe. Prof. Ndalichako

Pia alielezea namna Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inatekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi wa Vijana ambapo kupitia program hiyo zaidi ya vijana 87,845 wamepatiwa mafunzo ya kukuza ujuzi na stadi za kazi katika fani mbalimbali.

Aidha, Waziri Ndalichako alitoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali na kuhakikisha kuwa wanakuwa wepesi wa kutafuta taarifa hasa zinazowahusu.

“Niwasihi vijana kuwa wazalendo na wenye maadili kwa kufuata silka za kitanzania na kuhakikisha amani nchini, msitumie nguvu kazi hiyo vibaya kwani Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana mipango mizuri juu ya Vijana na kamwe msimuangushe,” alisema Waziri Ndalichako

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda alitumia fursa hiyo kuwasihi viongozi wa dini na makundi mengine mbalimbali ikiwemo ya Vyuo na elimu ya Kati kuhakikisha wanaendelea kuunga mkono vijana ili waweze kufanikisha malengo waliyonayo.

Akizungumza awali Mwanzilishi wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT), Bw. Isaac Mpatwa alieleza kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na serikali katika kuwajenga vijana kwenye misingi imara itakayowawezesha kuwa na uwezo wa kupambana na changamoto mbalimbali za kijamii.

Kongamano hilo limehusisha viongozi kutoka taasisi za vijana na majadiliano yalikuwa yamejikita katika mada ambazo zinalenga kuwajenga vijana kimaadili na kuwa wazalendo kwa nchi yao.