Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

VIJANA MKOANI MOROGORO WATOA PONGEZI NA SHUKRANI KWA RAIS MAGUFULI


Vijana Wilayani Kilosa, Morogoro wamemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua yake madhubuti ya kufuta hati ya mashamba makubwa yaliyokua yanamilikiwa na watu wachache na kuyarejesha mikononi mwa wananchi.


Hayo yamesemwa leo mbele ya Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana Kazi na Ajira, Mhe Anthony Mavunde wakati wa mavuno ya mpunga katika shamba linalomilikiwa na Vijana wa Kampuni ya Agri-Ajira ambao ni wahitimu wa Chuo cha Kilimo Sokoine.

" Niwapongeze kwa uthubutu wenu na kazi kubwa mliyoifanya mpaka kufikia mafanikio makubwa, Kama Serikali tutawawezesha kimtaji kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili kupanua Kilimo chenu na kutoa ajira zaidi kwa Vijana, na kabla ya sijaondoka hapa nimtake Afisa kutoka Benki ya Kilimo kutoondoka hapa bila kuweka sawa andiko la mkopo na mahitaji ya vijana hawa," amesema Mh Mavunde.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi amewahakikishia vijana wilayani hapo kuwa Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega katika kuwapatia maeneo ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kuahidi kulifanyia kazi ombi la ekari 500 za ziada zilizoombwa na Kampuni hiyo ya vijana.


Awali wakisoma risala mbele ya Mhe Mavunde, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Charles Ibrahim ameishukuru Serikali ya Rais Magufuli kwa kuwapatia eneo la kilimo la ekari 50 ambapo pia amesema kama wataongezewa ekari 500 walizoomba basi wataongeza idadi ya ajira kutoka 200 kufikia 1000.