News
Vijana wanaotafuta ajira nje ya nchi wasitumie njia zisizo rasmi: Waziri Mkenda
Serikali imeendelea kutekeleza programu mbalimbali za kukuza ujuzi, kutoa mafunzo ya uanagenzi na kuwawezesha vijana kupata uzoefu wa kazi, pamoja na kuwaunganisha na fursa za ajira ndani na nje ya nchi. Hatua hiyo inalenga kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na kuongeza uwezo wao wa kujiajiri na kuajiriwa.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2026, yaliyofanyika Oktoba 10, 2026, katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mkenda amewataka vijana wanaotafuta ajira nje ya nchi kutumia njia rasmi zinazotambuliwa na Serikali, akisisitiza umuhimu wa kufahamu haki na wajibu wao kabla ya kusafiri. Ameeleza kuwa fursa za ajira za kimataifa zinapaswa kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi na kujenga maisha bora, badala ya kuwaweka katika mazingira ya unyonyaji, udanganyifu au hatari.
Aidha, Prof. Mkenda amewahimiza vijana kufuatilia kwa karibu taarifa za fursa za ajira, mafunzo, programu za maendeleo, masomo, ubunifu na ujasiriamali zinazopatikana ndani na nje ya nchi. Amesema fursa hizo zinaweza kupatikana kupitia ushirikiano wa Serikali na nchi jirani, taasisi za kimataifa pamoja na sekta binafsi, hivyo vijana wanapaswa kuwa na utayari wa kujifunza na kutumia ipasavyo fursa zinazojitokeza.
“Vijana msisubiri fursa ziwafuate, tafuteni taarifa, andaa maombi yenye ubora na tumieni mifumo iliyo rasmi,” amesema Prof. Mkenda, akisisitiza umuhimu wa vijana kuwa wabunifu, wenye bidii na wanaojituma katika kutafuta nafasi za kujiendeleza kitaaluma na kiuchumi.

.jpeg)

