Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waajiri Sekta ya Umma na Binafsi wahamasishwa kuwajengea uwezo watumishi wao


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi , Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amewataka Waajiri Sekta ya umma na binafsi kujenga utamaduni wa kuwajengea uwezo Watumishi wao ili waweze kuelewa vyema taratibu, miongozo, sheria na kanuni zinazosimamia ajira zao.

Naibu Waziri Katambi amesema hayo jijini Mwanza wakati akifungua semina ya waajiri na viongozi wa matawi ya TUGHE iliyolenga kuwajengea uelewa wa kuondoa migogoro mahala pa kazi.

Mhe. Katambi amesema kuwa, makosa ambayo yamekuwa yakifanywa na wafanyakazi ni kutokana na kutojua Sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya utumishi, hivyo kuwajengea uwezo kutaondoa changamoto za migogoro isiyokuwa na tija kwenye kazi.

“Mara nyingi wafanyakazi wanatenda makosa kwa kutojua Sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya kiutumishi, hivyo mafunzo haya yaliyowakutanisha Wawakilishi wa Wafanyakazi na Wawakilishi wa Waajiri, Maafisa Utumishi, Maafisa Tawala na Wanasheria wa Taasisi yatatoa fursa ya kuwajengea uelewa wa kuimarisha amani katika mahala pa kazi,” alisema

Ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kuhakikisha wafanyakazi wanapata fursa ya kujiunga na kuanzisha Chama cha wafanyakazi wanachokipenda kwa kuwa na uhuru wa kujumuika ikiwa ni haki ya msingi kwa mfanyakazi mahali pa kazi na katika kuchochea tija na ufanisi.

Pia, Naibu Waziri Katambi amesema kuwa suala la nyongeza ya kima cha chini cha Mishahara ya Wafanyakazi katika Sekta Binafsi lipo katika hatua za mwisho kukamika na hatimaye kutangaza rasmi kima cha chini cha mishahara ya wafanyakazi wa sekta binafsi kama alivyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za Mei Mosi 2022.