Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waajiri watakiwa kuzingatia Sheria na kutoa Mikataba ya Kazi


Waajiri nchini wametakiwa kuzingatia Sheria na kutoa mikataba ya kazi kwa kazi zinazostahili mikataba badala ya kuwafanyisha watu kazi kama vibarua kwa kazi ambazo wangeweza kupata mikataba ya kazi.

Rai hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Disemba 2, 2022 wakati wa hafla ya utoaji Tuzo za Mwajiri Bora wa Mwaka 2022 zinazoratibiwa na Chama cha Waajiri Nchini (ATE) iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Aidha, amewasisitiza waajiri kuzingatia Sheria zilizopo kuhusu ajira kwa wageni ikiwemo kuhakikisha nafasi zisizo za kitaalamu au ambazo utaalamu wake unaweza kupatikana hapa nchini hazitolewi kwa wageni.

Vilevile, amewataka waajiri kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kulingana na wakati ikiwa ni pamoja na kutoa posho, tuzo na motisha mbalimbali ili kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi bora katika taasisi, kuwapandisha vyeo na kuwapatia stahili zinazoendana na nafasi zao.

Pia, Makamu wa Rais ameagiza Wizara ya Kazi kutoa elimu kwa wafanyakazi na waajiri nchini ili waweze kujua haki zao pamoja na kuhakiki aina ya mikataba inayotolewa kwa lengo la kukidhi vigezo vyote muhimu ikiwa ni pamoja na kuainisha wajibu na haki za mwajiri na waajiri kwenye masuala ya afya, likizo, ulemavy, mafao na migogoro.

Sambamba na hayo, amewataka waajiri kutumia tuzo hizo kama chachu ya kuboresha mazingira ya mahala pa kazi na kuhamasisha utendaji wenye tija kwa manufaa ya Taasisi zao na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewaeleza Waajiri kuwa Serikali imekamilisha upangaji wa kima cha chini cha Mshahara katika sekta binafsi na kima hicho tayari kimetangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 687 la tarehe 25 Novemba, 2022.

"Nitumie fursa hii kuwafahamisha rasmi kwamba kima hicho kitaanza kutumika rasmi kuanzia tarehe 01/01/2023. Ikumbukwe kwamba kwa miaka 9 iliyopita toka mwaka 2013 kulikuwa hakuna tamko rasmi la kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi,"