Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Wadau wa Maendeleo ya Vijana waaswa kutoa fursa za Ajira kwa Vijana


✅ Wasisitizwa kuwekeza katika Ajira za Vijana kwa Maendeleo ya Taifa.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Bi. Zuhura Yunus ametoa wito kwa sekta binafsi, Asasi za kiraia na Wadau wa Maendeleo kushirikiana na Serikali katika kufungua fursa za Ajira kwa Vijana.

Aidha, amesema vijana wa Tanzania wamekuwa wakionesha mchango mkubwa katika kuchangia maendeleo ya taifa, hivyo ni muhimu wadau hao wakaibua na kulea vipaji, kukuza ubunifu na kuendeleza ujuzi kwa vijana ili kuongeza nafasi za ajira na kukuza uchumi wa Taifa.

Naibu Katibu Mkuu, Zuhura amebainisha hayo Agosti 12, 2025 wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa iliyofanyika katika ukumbi wa Mabele uliopo Mabeyo Complex, Jijini Dodoma.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kuwezesha vijana kushiriki katika shughuli za Maendeleo ikiwemo Maboresho ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana (2007), Toleo la Mwaka 2024, Sera ya Ajira na mikakati inayolenga kukuza ujuzi wa vijana ili kuwawezesha kuhimili ushindani katika soko la Ajira.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kusimamia na kutekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi kwa Vijana, pia kuwezesha Vijana Kiuchumi na vile vile Mpango wa Taifa wa Ajira ambao umeunganishwa na sekta binafsi ili kufungua fursa za ajira ndani na nje ya nchi.