News
WAKULIMA 258 wanufaika na Mafunzo ya Ukuzaji Ujuzi
SingidaOfisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu yahitimisha mafunzo ya ukuzaji Ujuzi kwa Mkoa wa Singida yaliyolenga kuboresha mbinu za kilimo na kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la Alizeti.
Mafunzo hayo yamewanufaisha wakulima na wasindikaji wadogo 258 kutoka kwenye maeneo yenye shughuli za kilimo cha Alizeti kwa kuwaleta pamoja kwa lengo la kubadilishana maarifa na kuongeza ujuzi wa teknolojia mpya.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Mtaalam kutoka Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi Bw. Abiud Shumbusho amewashukuru wakulima wa Alizeti Mkoa wa Singida kwa kujitokeza kwa wingi na kwa ushirikiano waliouonyesha kipindi chote cha mafunzo yalofanyika siku 4 kwenye Wilaya ya Ikungi, Singida Mjini, Iramba na Mkalama.
“Leo tarehe 13 Novemba 2025, tunahitimisha mafunzo haya kwa mkoa huu hapa wilayani Mkalama hata hivyo lakini tunatarajia kuendelea na mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa Mkoa wa Mbeya na Iringa. Nitoe wito mafunzo haya mliyoyapata mkayatumie vizuri kwenye mashamba yenu na biashara zenu ili ziweze kuongeza uzalishaji na kipato kiujumla.” alisema Shumbusho.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku nne katika Wilaya za Ikungi, Singida Mjini, Iramba na Mkalama yameratibiwa kwa kushirikiana baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ambayo inatoa utaalamu wa juu ya faida na umuhimu wa zao la alizeti, viwango vya ubora na usalama, mbinu bora za usimamizi wa alizeti baada ya mavuno, uongezaji thamani zao la alizeti na mbinu za kufikia masoko ya zao la alizeti na bidhaa zake.
Katika hatua nyingine wataalamu wa TARI pia wametoa elimu ya vitendo kwa washiriki kuhusu, ubora wa udongo, uvunaji na usindikaji wa mafuta ya alizeti ambapo jumla ya Wakulima 258 wamefikiwa na mafunzo hayo.
Mmoja wa watafiti hao kutoka TARI Bwa. Emmanuel Mwenda amesema Mafunzo hayo yametolewa kwa wakulima wa alizeti kwa ajili ya kuwaongezea Ujuzi wakulima na wasindikaji wadogo,tunafahamu umuhimu wa zao hili ndio maana tunawaongezea ujuzi ili tuwe na malighafi zenye ubora ambao umekusudiwa.
“Badala ya wakati wote kuuza Mafuta pekee pia wanaweza wakaongeza thamani na kupata bidhaa nyengine ambazo zinapatikana katika zao hilo ili kuweza kuongeza kipato zaidi kupitia mbinu za kisasa ambazo ni mitandao ya kijamii ili waweze kujitangaza na kupata soko kubwa zaidi” amesema Mwenda.
Mmoja wa washiriki hao kutoka Mkoa wa Singida, Maria Gwila alisema “tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutupatia mafunzo haya, maana alizeti ndio zao kubwa mkoani Singida, kiukweli wengi wetu tulikuwa hatuna elimu kutumia teknolojia kama chanzo cha kutunufaisha kiuchumi ila mafunzo haya yametuongezea ujuzi ambao tunaamini tukiutumia vyema utatusaidia kuongeza kipato na uzalishaji pia” alisistiza Gwila.
Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira,Vijana,na Wenye Ulemavu inatekeleza programu ya ukuzaji ujuzi kwa wakulima kwa lengo la kuwezesha nguvu kazi ya taifa, kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
