Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

​Wakulima Kuweni Mabalozi wa Mafunzo ya Kukuza Ujuzi


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Zuhura Yunus amewataka wakulima Wadogo na wasindikaji wa zao la Zabibu kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya ili kukuza ujuzi wa kuongeza thamani ya mazao kwenye mnyororo wa mazao ya kilimo.

Zuhura Yunus ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wakulima na wasindikaji wadogo katika sekta ya kilimo leo (21 Oktoba, 2025) Jijini Dodoma yanayolenga kuongeza weledi na ujuzi kwa wakulima wapatao 1,000 nchini.

“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji , kuimarisha njia za za utendjai kazi ili kuongeza ubora wa bidhaa na kutoa huduma bora zaidi katika sekta ua kilimo” alisema Naibu Katibu Mkuu Zuhura Yunus.

Aidha, amesema wakulima na wazalishaji Wadogo huchangia katika uzalishaji wa mazao ya chakula nchini na kutoa malighafi kwa viwanda lakini wamekuwa na changamoto ya upungufu wa ujuzi wa mnyororo wa thamani ndio maana Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeandaa mafunzo haya kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo.

Wakizungumza kwa niaba ya washiriki Bi. Mary Uguzi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapatia ujuzi wenye tija, Naye Noha Madeje amesema kuwa kupitia mafunzo waliyopata wamejifunza vitu vingi katika utengenezaji bora wa wine lakini pia wanufaika hao wameiomba Serikali kuendelea kuwapatia mikopo itakayowawezesha kukuza biashara zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Thomas Bwana ambaye anaongoza timu ya wataalam kufundisha wakulima hao aliwashauri kuwa watumie elimu na ujuzi watakao upata Kwenda kuwafundisha wenzao ili tija inayokusudiwa iweze kupatikana.

Dkt. Bwana aliongeza kusema kuwa TARI imejipanga kuhakikisha matokeo ya tafiti wanazozifanya zinawafikia na kuwasaidia wakulima na wasindikaji wa bidhaa za kilimo nchini ili tija ipatikane na kuchangia ukuaji wa Uchumi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi Alana Nchimbi alieleza kuwa mafunzo hayo baada ya kufunguliwa leo yatatolewa katika mikoa minne na aina mazao yatakayohusika kwenye mafunzo hayo ni Dodoma (zabibu), Singida (alizeti), Iringa (nyanya na mchicha lishe) na Mbeya (maharage na parachichi) ambapo jumla ya wakulima 250 kwenye mikoa hiyo watanufaika.

Alana aliongeza kuwa Ofisi hiyo inaratibu mafunzo hayo kwa kushirikana na wadau ili kuwezesha nguvukazi katika sekta mbalimbali kupata ujuzi stahiki kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi (Up-Skilling training) kwa mwaka wa fedha 2025/2026.