Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Wataalam wa Kinga ya Jamii wakutana Morogoro


Wataalam wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii nchini wamekutana kujadili na kuweka mikakati ya kuviwezesha vikundi kazi, ili kuhakikisha jamii inafikiwa na huduma za kinga ya jamii kwa lengo la kuongeza ustawi wa jamii.

Akizungumza katika kikao kazi hicho cha kwanza 26 Novemba 2026, Mkurugenzi wa Kinga ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mh. Festo Fute, alisema kikao hicho kinalenga kujadili utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii kupitia vikundi kazi vya Kinga ya Jamii(Thematic Working Groups).

Fute aliendelea kusisitiza kuwa Ofisi imeandaa utaratibu wa utekelezaji wa sera hiyo na imeanzisha vikundi kazi vinne. Vikundi hivyo ni pamoja na Misaada ya Kijamii (Social Assistance), Mifuko ya Uchangiaji (Social Insurance), Huduma za Ustawi wa Jamii (Social Welfare) na Uzalishaji Jumuishi (Productive Inclusion). Alieleza kuwa kila kikundi kitawasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake katika kikao hicho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Misaada ya Kijamii katika Ofisi hiyo, Novatus Msemwa, alisema washiriki wa kikao hicho ambao wametoa maoni yao, Ofisi imeyachukua na yatakayosaidia kuimarisha utekelezaji wa sera hiyo. Alieleza kuwa utekelezaji wa sera unahusisha wizara zote na kwamba, katika hatua ya awali, wizara kumi zinaendelea kutekeleza afua mbalimbali za kinga ya jamii.

Kikao hicho cha siku mbili kinafanyika katika ukumbi wa Cate Hotel, Morogoro, na kinaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, ikihusisha wawakilishi wa wizara za kisekta, mifuko ya hifadhi ya jamii, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), vyuo vikuu, Benki Kuu ya Tanzania na mashirika ya kimataifa, yakiwemo UNICEF, WFP na Benki ya Dunia.

Mwisho