News
Waziri Sangu awataka makamishna wa CMA kuja na mikakati ya kupunguza migogoro ya kazi
✅ Aitaka Kamati ya Huduma Muhimu kuchunguza migogoro katika sekta za huduma muhimu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amewataka Makamishna wapya wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kuja na mikakati ya kupunguza migogoro ya kazi inayofikishwa katika Tume hiyo, pamoja na kutoa elimu kuhusu utatuzi wa migogoro katika maeneo ya kazi.
Ametoa wito huo leo, Novemba 26, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Makamishna wa Tume na Kamati ya Huduma Muhimu, inayofanyika jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa NSSF.
Aidha, amemtaka Mwenyekiti wa Bodi ya CMA kuhakikisha inaimarisha utoaji wa huduma kwa njia za kidijitali, ili kurahisisha upatikanaji wa haki na huduma mbalimbali za Tume.
“Nimejulishwa kwamba ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa CMA kupata kiongozi ambaye ni Jaji, na tunajua Mahakama inafanya vizuri sana katika utoaji wa huduma, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali. Hivyo, tunatarajia mafanikio yaliyopatikana Mahakamani tutayashuhudia yakitokea pia CMA,” amesema Waziri Sangu.
Vilevile, amewapongeza Makamishna waliomaliza muda wao kwa mchango wao katika kuimarisha utendaji wa Tume, hususan kuanza kutumika kwa mfumo wa e-Utatuzi ambao hadi sasa umesajili jumla ya migogoro 3,885.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya CMA, Mhe. Jaji Mstaafu Wilfred Dyansobera, amemshukuru Waziri Sangu kwa kuwakumbusha wajibu wao na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan huku akiahidi ushirikiano katika kuhakikisha Tume inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Naye, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Bw. Idris Mvura, ameiomba Serikali kuendelea kuiwezesha CMA kupata bajeti ya kutosha ili kutekeleza majukumu yake.
.jpeg)



