Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Watanzania kunufaika na fursa za ajira nchini Oman


Watanzania wataanza kunufaika na fursa za ajira nchini Oman baada ya kuhitimishwa kwa majadiliano ya makubaliano ya uwili wa kushirikiana katika masuala ya ajira.

Kukamilika kwa majadiliano hayo kunatoa fursa ya kusainiwa kwa mkataba wa mpango huo wakati wowote kuanzia sasa.

Akizungumza wakati wa majadiliano hayo Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu amesema mpango huo wa ajira unahusu fursa zilizopo katika nchi zote mbili.

Amesema makubaliano hayo yana manufaa makubwa kwa Tanzania katika kuhakikisha Watanzania wanapata ajira zenye staha na zinazoheshimu haki za binadamu nchini Oman.

Balozi wa Oman nchini, Saud Al-Shidhani amesema Tanzania na Oman zitahakikisha zinalinda haki za wafanyakazi watakaokwenda kufanya kazi kwenye nchi hizo kama walivyokubaliana.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab alisema walikutana jana kwa lengo la kurasimisha makubaliano yatakayosaidia kusainiwa kwa mkataba utakaoruhusu Watanzania kwenda kufanya kazi nchini Oman.

Katibu Mkuu (Kazi na Uwezeshaji) Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Maryam Juma Saadalla amesema makubaliano hayo yatanufaisha pande zote mbili za Muungano kwa Watanzania kwenda kufanya kazi Oman.

Pia amesema makubaliano hayo yatasaidia kufikia lengo la kuwa na ajira milioni nane ifikapo mwaka 2025 kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM) inavyoelekeza.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Joseph Nganga amesema kupitia makubaliano hayo watawalinda wafanyakazi watakaokwenda kufanya kazi pande zote mbili dhidi ya aina yoyote ya unyonyaji, ubaguzi, uzalilishaji wa kingono, unyanyasaji, kulazimishwa kazi na mambo mengine yanayofanana na hayo.