Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Watoa huduma za kifedha watakiwa kufikisha huduma kwa vijana


Watoa huduma za kifedha nchini wametakiwa kutumia fursa na huduma wanazotoa kubuni mbinu mpya zitakazo wafikia vijana wengi kwa kuwawezesha kupata mikopo yenye riba nafuu itakayowasaidia kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Rai hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati akifungua wa Maadhimisho ya pili ya Wiki ya Huduma za Kifedha yanayofanyika katika viwanja vya Rock City Mall, jijini Mwanza, Novemba 24, 2022.

Ameeleza kuwa, huduma za kifedha ni chachu ya maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi, hivyo ni vyema taasisi za kifedha wakatanua wigo wa huduma za kifedha zitakazo wafikia vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya Taifa.

“Mheshimiwa Rais hivi karibuni alitangaza idadi ya watu nchini ambayo imefikia milioni 61.74 na vijana ndio sehemu kubwa ya taifa letu, hivyo taasisi zetu za kifedha zisione vijana ni soko gumu, bali wakabuni mbinu mpya na bunifu (creative interventions) zitakazo wafikia vijana wengi hapa nchini,”

Ameongeza kuwa, huduma za kifedha ni muhimili muhimu kwa uzalishaji, masuala ya kibiashara, uwekezaji na kukuza uchumi.

Sambamba na hayo, ametoa wito kwa watoa huduma za kifedha nchini kutazama upya masharti ya mikopo ili kuwezesha wananchi kukopa kwa riba ndogo.

Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Idara ya Hifadhi ya Jamii pamoja na Taasisi zilizo chini yake ambazo ni Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inashiriki Maonesho hayo ikiwa ni: WCF, PSSSF na NSSF.