Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Mkuu aeleza namna Serikali Ilivyodhamiria Kuwawezesha Vijana


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema serikali imedhamiria kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi kupitia programu mbalimbali ikiwamo mafunzo ya uanagenzi ili kupata ujuzi wa kujiajiri.

Mhe. Majaliwa ameyasema hayo leo bungeni katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu , alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum (CCM) Mhe. Ng’wasi Kamani ambaye amehoji mkakati wa serikali wa kuendelea kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili kutunisha mfuko wa maendeleo ya vijana ili wajikwamue kiuchumi.

Waziri Mkuu amesema serikali inatekeleza programu za kuwawezesha vijana na imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya mfuko huo uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu.

“Kila mwaka serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya mfuko huu kuanzia mwaka 2017 zilitengwa Sh.Bilioni 1 na tukaongeza tena na tunatoa kwa vijana wanaokidhi vigezo kupitia Halmashauri, tumeunda mfuko maalum na tuna mwongozo wa kuendesha mfuko, huwa tunatoa fursa kwa wadau pia kuuchangia mfuko huu,”amesema.

Mhe. Majaliwa amesema mpango wa serikali ni kuhakikisha vijana wanawezeshwa kupitia mfuko huo na kuhamasisha vijana kuchangamkia fursa hiyo na kuunda vikundi.