Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Mkuu amewataka Wananchi kuendelea Kutunza Mazingira


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

"Tanzania ni moja ya nchi zinazoathiriwa na changamoto za uharibifu wa mazingira unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kupitia shughuli zisizo endelevu za kibinadamu zikiwemo uvamizi wa maeneo tengefu, vyanzo vya maji na matumizi holela ya mbolea zenye kemikali na viuatilifu, ufugaji wa kuhamahama unaojumuisha makundi makubwa ya mifugo, ukataji holela wa miti kwa ajili ya kuni, uchomaji wa mkaa na upanuzi wa mashamba na makazi, uchomaji moto ovyo wa misitu na mbuga, uchimbaji wa madini usio endelevu na uvuvi haramu, uvunaji haramu wa mikoko na kuenea kwa viumbe vamizi," amesema

Waziri Mkuu, Majaliwa ametoa rai hiyo Aprili 1, 2023 wakati akizungumza na wakazi wa Mtwara na mikoa ya jirani waliofika kushuhudia uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa uliofanyika kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona, katika Manispaa ya Mtwara.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kulinda mazingira na vyanzo vya maji kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 ambayo imeweka masharti yanayozuia uharibifu na uchafuzi wa mazingira kutokana na shughuli za kiuchumi na kijamii ili kuwa na uhifadhi endelevu wa Mazingira.

Ameongeza kuwa, wakati akifungua Siku ya Mazingira Duniani - Jijini Dodoma, Juni 5, 2022 alitoa maelekezo 15 kwa ajili ya utunzaji wa mazingira ambayo ni: Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha Mpango kabambe wa Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira unakuwa sehemu ya vipaumbele vya bajeti vya kila mwaka kwa kipindi chote cha utekelezaji wake wa miaka kumi; Wizara za kisekta, Mikoa na Halmashauri, zihakikishe Mpango huo unajumuishwa katika mipango na Bajeti zao; Kila Halmashauri kuhakikisha maeneo yaliyoharibiwa yanarejeshwa kwa kupandwa miti.

Pia, Halmashauri zihakikishe zinatekeleza vema programu ya kitaifa ya upandaji miti 1,500,000 ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa ya kijani; Wizara, Taasisi, Mashirika ya Serikali na binafsi yanayotumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia au shughuli nyingine za uzalishaji zianze kutumia nishati mbadala; halmashauri zihakikishe matukio ya uchomaji ovyo misitu yanadhibitiwa; pamoja na Taasisi za utafiti na vyuo vya elimu ya juu ziendelee kufanya tafiti za nishati mbadala ili kuondokana na utegemezi wa nishati ya kuni na mkaa kwa kupikia.

Vilevile kila Halmashauri kuweka utaratibu wa kuhakikisha taka zinatenganishwa na kukusanywa; Mamlaka zinazo husika na usimamizi wa mifereji ya maji ya mvua mijini kuhakikisha mifereji inasafishwa ili kupunguza matukio ya mafuriko mijini.

Pia, Halmashauri zihakikishe maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya misitu ya mijini katika mamlaka zao hayabadilishwi matumizi wala kuvamiwa; Sekta zinazohusika zihakikishe kuwa ardhi na uoto hususan wa asili katika vyanzo vya maji, milima iliyo katika maeneo yao inalindwa na kuhifadhiwa ili kuzuia mmomonyoko wa udongo na kukauka kwa vyanzo hivyo vya maji; sekta zinazohusika na usimamizi wa shughuli za umwagiliaji mashamba kuhakikisha matumizi sahihi ya maji yenye kuzingatia uhifadhi na ulinzi wa mazingira; Taasisi za utafiti na vyuo vya elimu ya juu kufanya tafiti kuhusu kuzuia na kudhibiti kuenea kwa viumbe vamizi vinavyochangia uharibifu wa mazingira nchini; Mamlaka ambazo zinahusika na usimamizi wa hifadhi za wanyamapori kudhibiti matukio ya ajali za barabarani kwa Wanyamapori; na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na mamlaka zingine kuhakikisha zinadhibiti shughuli za binadamu pamoja na uvamizi katika maeneo ya mapito ya wanyamapori (shoroba) ili kupunguza uharibifu wa mazao, mali na binadamu kupoteza Maisha kutokana na kuwepo mwingiliano wa wanyama na binadamu.

Mheshimiwa Majaliwa, amesema Serikali kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2023 itapata taarifa kuhusu utekelezaji wa maagizo hayo.

Hali kadhalika, Waziri Mkuu Majaliwa amewasisitiza Watanzania wote kuzingatia lishe bora ili kujenga jamii yenye afya na nguvu kazi imara kwa maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavy Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023, unazingatia umuhimu wa kuhifadhi Mazingira na utunzaji wa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa viumbe hai na Uchumi wa Taifa.

"Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na ujumbe maalum kila mwaka kulingana na vipaumbele vya Taifa letu na Dunia kwa ujumla, Ujumbe wa mwaka huu unalenga kuwaelimisha wananchi juu ya athari za mabadiliko ya Tabia nchi yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira.

Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 zinaongozwa na kauli mbiu isemayo: "Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa viumbe hai na Uchumi wa Taifa".