Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Mkuu awapongeza Watumishi Ofisi ya Waziri Mkuu


*Awataka waendelee kufanya kazi zitakazoleta matokeo chanya

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu waendelee kufanya kazi Weledi, Ubunifu na bidii ili kuchochea maendeleo ya haraka yenye matokeo chanya kwa Watanzania.

Waziri Mkuu amesema hayo jana usiku (Jumatano, Aprili 19, 2023) wakati akizungumza na watumishi wa ofisi hiyo na taasisi zilizo chini yake kwenye hafla fupi ya futari aliyoiandaa kwa ajili yao, Mlimwa, jijini Dodoma.

Aidha Mheshimiwa Majaliwa amemuahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kufanya kazi ambayo iteleta matokeo chanya kwenye masuala mbalimbali ya kimaendeleo "Sisi watumishi tuendelee kufanya kazi hii nzuri ya kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali".

"Nitumie fursa hii kuwapongeza kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa shughuli za serikali. Natoa pongezi kwa uwajibikaji mzuri na pia naungana nanyi kumuahidi Mheshimiwa Rais wetu kuwa tutafanya kazi bidii zaidi," amesema.

Waziri Mkuu amewataka watumishi hao waendelee kuhakikisha Serikali inapata mafanikio. "Tuna jukumu la kumwezesha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kusimamia miradi yote ya maendeleo. Sisi ndiyo tunapaswa kuratibu na kusimamia miradi ili ifanikiwe" amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi wa Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Jenista Mhagama amewataka watumishi hao waendelee kutunza heshima ya Ofisi pamoja na kumuwezesha Mheshimiwa Waziri Mkuu kumsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan majukumu ipasavyo.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi wa Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amesema watumishi wanapaswa kuendelea kufanya kazi upendo ukarimu na mshikamano ili nchi uweze kufanikiwa.

Watumishi walioshiriki futari hiyo wanatoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu zikiwemo OSHA, WCF, NSSF, PSSSF, TACAIDS, DCEA na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Mbali na watumishi, Waziri wa Nchi (OWM-SBU), Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi (OWM-KVAU), Prof. Joyce Ndalichako wengine waliohudhuria ni Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi, wakuu wa taasisi, wakuu wa idara na vitengo.