Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Mkuu mgeni rasmi Uzinduzi Mafunzo ya Uanagenzi Mbeya


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Uzinduzi wa Programu ya Mafunzo ya Uanagenzi kwa Awamu ya Tatu tarehe 2 Agosti, 2021 katika Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokutana na Waandishi wa Habari kwenye Ukumbi wa Chuo cha MUST kwa lengo la kutoa taarifa kwa umma kuhusu tukio la uzinduzi huo na shughuli zitakazoambatana na uzinduzi.

Kaulimbiu katika uzinduzi huu ni “NGUVUKAZI YENYE UJUZI STAHIKI, MSINGI IMARA KATIKA MAENDELEO YA TAIFA”. Kaulimbiu hii inatokana na dhana nzima ya masuala ya ajira, inatoa fursa kwa kila mmoja kuweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, ambapo anahitaji kuwa na ujuzi stahiki unaohitajika kufanya shughuli husika.

Akifafanua kuhusu programu hiyo, alieleza kuwa Ofisi yake imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi nchini kwa kuhakikisha inawafikia vijana wengi zaidi katika Mikoa yote nchini ambapo Programu hii ina vipengele vikuu vinne (4) ambavyo ni mafunzo uzoefu wa kazi kwa wahitimu (internship), urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo (RPL), mafunzo ya uanagenzi (apprenticeship) na mafunzo ya kuhuisha ujuzi kwa wafanyakazi (skills upgrading).

Mafunzo ya Uanagenzi yanahusisha mhusika kutumia asilimia 40 ya muda wake kwa masomo ya nadharia darasani na asilimia 60 ya muda wake kwa masomo ya vitendo sehemu ya kazi. Mafunzo haya ni ya muda wa miezi sita na yalianza kutolewa Mwezi Juni, 2021 na yanatarajiwa kukamilika Mwezi Disemba, 2021 ambapo Serikali inayafadhili kwa asilimia 100 kulingana na kibali kilichotolewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

“Tangu kuanzishwa kwa Programu ya kukuza ujuzi nchini, mafunzo ya uanagenzi yamefanyika awamu mbili ambazo jumla ya vijana 28,941 wamenufaika. Awamu hii ya tatu yanatolewa kwa vijana 14,440 na yanafanyika kupitia vyuo 72 katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara”,alisisitiza Waziri Mhagama

Aliongezea kuwa mafunzo haya yanatolewa katika fani mbalimbali kama vile ufundi umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa jua, useremala, ufundi magari, umeme wa magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, utengenezaji wa vifaa vya aluminiam, upishi, uhudumu wa hoteli na vinywaji, ushonaji, uchenjuaji wa madini, ufundi bomba, ufundi uashi, uwekaji wa terazo na marumaru, ufundi viyoyozi na majokofu.

Aidha hadi Disemba, 2021 kutatarajia kuwa na jumla ya wanufaika wa kupitia programu zote nne kufikia 80,320. Kati ya hawa, vijana 43,381 ni kupitia mafunzo ya uanagenzi, vijana 20,334 kupitia mafunzo ya urasimishaji ujuzi, vijana 5,975 kupitia mafunzo ya uzoefu wa kazi (internship), vijana 9,080 (100 nchini Israel) kupitia mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia kitalu nyumba (green house), na vijana 1,550 kupitia mafunzo ya kukuza ujuzi wa waajiriwa (skills upgrading).

Sambamba na uzinduzi huo Mhe.Waziri Mkuu anatarajiwa kuwa na shughuli mbalimbali zitakazofanyika Mkoani Mbeya.

“Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atatembelea vyuo vinavyotoa mafunzo ya Uanagenzi Jijini Mbeya, atatembelea Kyela Polytechnic College, VETA Busokelo, VETA Mbeya, Chuo cha Ufundi cha Magereza Ruanda na Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) ili kuona na kukagua namna mafunzo yanavyotolewa, na kuweza kuzungumza na vijana wanaopata mafunzo husika”,alisema Waziri Mhagama.

Akihitimisha Waziri alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi wote kuzingatia suala zima la afya hususan kipindi hiki ambapo tuna mlipuko wa COVID 19 nchini kwa kuchukua tahadhari zote huku wakizingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wetu nchini.

“Ninapenda kutoa wito kwa wananchi watakaoshiriki kwenye tukio la uzinduzi huu kuchukua tahadhari zote ikiwemo kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono na kunawa mikono kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya ili kujilinda na kulinda wengine”.