Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

​WAZIRI MKUU: UJENZI MJI WA SERIKALI UMEONGEZA FURSA ZA AJIRA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema ujenzi wa mradi wa Mji wa Serikali unaondelea jijini Dodoma umesaidia kuongeza fursa za ajira na maendeleo kwa wananchi kwa kuwawezesha kufanya shughuli zinazowaingizia kipato.

Mhe. Waziri Mkuu ameeleza hayo leo Septemba 5, 2022 mara baada ya kukamilisha ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan inafanya jitihada za ushirikishwaji wananchi katika miradi ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Tumeendelea kuona jitihada za Mhe. Rais Samia za kutekeleza miradi ya maendeleo. Jitihada hizo zinasaidia kutatua changamoto za ajira nchini.Katika mradi huu wapo vijana mafundi waliopata ajira lakini pia yapo makundi ya wanawake na wanaume wanaofanya biashara hali inayo wawezesha kujiongezea kipato”

Aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu amewataka vijana wanaofanya kazi katika mradi huo wa ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, kuhakikisha ujuzi walioupata wanautumia katika kutekeleza miradi mingine kama hiyo, kwa kuwa hadi kukamilika kwa mradi huo watakuwa na wanaoujuzi wa kutosha.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa mradi huo wa ujenzi wa Mji wa Serikali umekuwa ukizalisha ajira za moja kwa moja na mabazo sio za moja kwa moja.

“Katika Ujenzi wa Majengo yote ya Serikali unaoendelea hapa Mtumba, ajira 120 zinazalishwa kwa siku, ambapo wananchi wanaoshiriki katika ujenzi huu wanaweza kujikwamua kiuchumi kupitia ajira hizo”