News
Waziri Nanauka: Vyuo Vikuu ni Maabara ya Fikra kwa Vijana
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka amewasihi vijana katika ngazi ya vyuo vikuu nchini kutumia mijadala na masomo ili kuwa na uwezo wa kujenga hoja na fikra chanya za kukuza maendeleo ya Taifa na uzalendo.
Waziri Nanauka amesema hayo wakati akizungumza na vijana pamoja na viongozi wa serikali ya wanachuo Kikuu cha Dar es Salaam (05 Desemba 2025) alipowatembelea na kuzungumza nao ambapo amesema kwa sasa asilimia 65 ya watanzania ni vijana chini ya miaka 35 na hivyo kuhitaji kujumuishwa kwenye mipango ya maendeleo.
Amefafanua kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuunda wizara ya vijana ili iwe maalum kwa ajili ya kufikisha sauti za vijana zisikike na Serikali ipate fikra na mawazo yao kujumuishwa kwenye mipango ya maendeleo ya nchi.
“Nahitaji kusikia mawazo yenu vijana wa vyuo vikuu na ndio maana nimefika hapa kuzungumza nanyi. Natambua vyuo vikuu ni maabara ya fikra, hivyo ni sehemu mahsusi ya kujenga hoja na mijadala yenye faida kwa jamii.
Tutaandaa midahalo ya vijana tuzungumze na kujadiliana kwa kirefu.” alisema Waziri Nanauka.
Akielezea uzoefu wake kwenye uongozi wa Serikali za wanafunzi, Nanauka ambaye naye alikuwa Mbunge wa DARUSO na mhitimu wa chuo hicho aliwasihi vijana kuwa mstari wa mbele katika kutumia mitandao ya kijamii kufikisha ajenda za maendeleo badala ya kuchapisha maudhui hasi au yaliyo kinyume cha sheria.
Katika hatua nyingine, Waziri Nanauka aliwaeleza vijana hao kuwa Serikali imesikia kilio chao kuhusu Katiba mpya ambapo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi katika uongozi wake atahakikisha nchi inarejesha mchakato hivyo kuwataka vijana kujiandaa kuchangia fikra zao juu ya nini Katiba iseme na iwe na masuala gani mahsusi kwa vijana.
Kwa upande Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. William Aangisye alisema katika kuhakikisha chuo kinaendana na mahitaji ya vijana kimeboresha mitaala yake hatua inayosaidia kutoa mafuzo yenye kuwajenga vijana kuwa mahili kwenye sekta mbalimbali mara baada ya kuhitimu.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho Mipango , Fedha na Utawala Prof. Bernadeta Killian alisema chuo hicho mwaka huu kimetoa jumla ya wanafunzi 11,000 waliohitimu fani mbalimbali ambapo vijana ndio Kundi kubwa linalokwenda kuingia kwenye ajira hivyo akashauri Wizara ya Vijana kuwa na program maalum za kuwafikia vijana vyuoni na kuzugumza kupata mawazo yao.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya wanafunzi Rais wa DARUSO, William Emanuel aliomba Serikali kuweka mazingiura wezeshi kwa vijana kushiriki kwenye mijadala ya kitaifa ili kuleta umoja miongoni mwa wasomi na vijana.
Waziri Nanauka anaendelea na ziara yake ya kukutana na vijana kwenye maeneo yao ya kazi na kuzungumza nao ili kuwasikiliza na kuwaeleza juu ya Wizara yao na nini itakachofanya kuleta utenganamno na wafanya vijana wachangie kwenye maendeleo ya Taifa.
