Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI NDALICHAKO AHAMASISHA WAAJIRI KUWA NA MKATABA WA HALI BORA KWENYE MAENEO YA KAZI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewataka waajiri nchini kuhakikisha wanakuwa na mikataba ya hali bora katika maeneo yao ya kazi ili kuongeza tija, kuepusha migogoro na kudumisha mahusiano mema.

Amesema hayo Agosti 26, 2022 katika hafla ya uwekaji saini Mkataba wa Hiari wa Hali Bora kati ya Menejimenti ya Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), na Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) Tawi la Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC).

Ameeleza kuwa, Makubaliano ya Mkataba wa Hali bora ni hatua ya utekelezaji wa Sheria za kazi hususani Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo uweka mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kitaasisi baina Wafanyakazi na Waajiri kwa lengo la kuboresha mazingira bora ya kazi, maslahi ya Wafanyakazi na kuleta tija mahala pa kazi.

“Ninafarijika kushuhudia waajiri kama kampuni ya TCC mnavyowajali wafanyakazi kwa kuchukua hatua hii ya kuwa na mkataba wa hali bora, ni kielelezo tosha mmedhamiria kuboresha maslahi ya Wafanyakazi na kuongeza hali ya kazi na uzalishaji,”

Aidha, Waziri Ndalichako ametoa rai kwa Waajiri kufunga mikataba ya hali bora na wafanyakazi ili waweze kuboresha maslahi ya Wafanyakazi wao, kuongeza tija, uzalishaji na kuweka bayana malengo na wajibu wa Wafanyakazi na mwajiri.