Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ndalichako awaalika Wadau Siku ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi Duniani Mkoani Morogoro


Kuelekea siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, amewaalika mkoani Morogoro waajiri na wafanyakazi kushiriki kikamilifu maadhimisho hayo ambayo huadhimishwa tarehe 28 Aprili kila mwaka.

Akiongea na waandishi wa habari leo tarehe 26 Aprili 2023 jijini Dodoma, Mhe. Prof. Ndalichako amesema maandalizi ya maadhisho hayo yamekamilika na kubainisha kuwa, kauli mbiu ya maadhimisho ya Mwaka huu ni "Mazingira Salama na Afya kazini ni Kanuni na Haki ya Msingi Mahali pa Kazi".

Amefafanua kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), kwa kushirikiana na wadau wa Utatu; Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA), Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Shirika la Kazi Duniani (ILO), kuelekea maadhimisho hayo, wataendesha kampeni maalum ya uhamasishaji Usalama na Afya mahali pa kazi yenye kuhusisha Mafunzo, Maonesho na Tuzo.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amefafanua kuwa kwa kushirikiana na OSHA na wadau wengine wataendelea kutoa taarifa muhimu ili kuendelea kuboresha mazingira salama mahali pa kazi.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Getrude Sima amesisitiza kuwa wataendelea kutoa msaada wa utalaamu kwa Tanzania ili iweze kutekeleza mikataba yote inayohusu usalama mahali pa kazi.Aidha, ameipongeza Tanzania kwa utekelezaji wa mikataba ya kazi na sheria za Usalama na Afya mahali pa kazi.

Awali akiongea katika Mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda amebainisha kuwa Taasisi hiyo itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, ili kuhakikisha magonjwa na ajali mahali pa kazi zinazuilika au zinapungua.