Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ndalichako Awaasa Waajiri Kuzingatia Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewaasa waajiri nchini katika sekta ya umma na binafsi kuendelea kuzingatia Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ili kuwezesha fidia kwa wafanyakazi waliopata changamoto kutokana na kazi kwa wakati.

Hayo yameelezwa na Waziri Ndalichako wakati wa ziara yake ya Kikazi alipotembelea Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) hii leo Januari 24, 2022 Jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu kwa kukagua utekelezaji wa majukumu katika Taasisi zilizopo chini ya Ofisi yake.

Alieleza kuwa, Mfuko huo umekuwa ukifanya kazi nzuri sana katika utekelezaji wa majuku yake ambayo ni kulipa fidia kwa wafanyakazi walioumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi, hivyo ni vyema waajiri nchini wakazingatia Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ili kuwezesha fidia kwa wafanyakazi kutekelezwa kwa wakati.

“Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni muhimu sana kwasababu ni kiashiria kuwa Serikali inatambua na kuthamini wafanyakazi katika sekta zote na ndio maana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza masuala ya fidia kwa wafanyakazi katika sekta mbalimbali,” alisema Waziri Ndalichako

Aliongeza kuwa, Mfuko huo ulianzishwa mwaka 2015 ambapo Julai 2022 mfuko huo utakuwa na miaka saba katika utekelezaji wa majukumu yake, hivyo umekuwa na tija kubwa kwa wafanyakazi nchini hususani katika kuwezesha fidia na kutoa ushauri nasaha kwa wafanyakazi pindi wanapougua ama kuumia kazini.

Sambamba na hayo, Mheshimiwa Ndalichako alipongeza Uongozi wa mfuko huo kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kutekeleza majuku yao, aidha aliwasihi kuendelea kushirikiana kwa lengo la kufanikisha malengo ya mfuko huo.

“Nimefarijika kuona watumishi waliopo katika Taasisi hii wanatambua umuhimu wa Mfuko huu katika kuhudumia wafanyakazi wa ufanisi na weledi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi alisema kuwa mafanikio ya mfuko huo ni uthibitisho wa uwezo mkubwa walionao watendaji katika kusimamia majukumu yao kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Emmanuel Humba alisema kuwa mfuko huo utaendelea kuhakikisha unafanisha dhima yake ili uweze kuwa mfano bora wa kuigwa na mifuko mingine.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alieleza kuwa Mfuko huo utahakikisha unaendelea kutoa huduma kwa ufanisi na tija ikiwa ni pamoja na kuhakikisha unawekeza kwa tija ili mfuko uwe endelevu na kustahimili ulipaji wa fidia kwa wafanyakazi.