Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ndalichako awapongeza wawekezaji kwa kutoa ajira kwa watanzania


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amewapongeza wamiliki wa viwanda wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kwa kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania kupitia uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi.

Ametoa pongezi hizo Leo tarehe 28 Oktoba 2022, alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku mbili (2) katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambapo ametembelea viwanda na maeneo ya kazi sita (6) yanayozalisha bidhaa vikiwemo vifungashio, vyombo vya majumbani, mabomba, vinywaji, taulo za kike na nyama.

“Nimehitimisha ziara katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Lengo la ziara hii ilikuwa ni kupata mrejesho wa utekelezaji wa Sheria za Kazi ikiwemo kuangalia ajira zinazozalishwa na wawekezaji wetu. Jambo la kufurahisha ni kwamba katika maeneo yote sita niliyotembelea nimeona zaidi ya ajira 3,000 zimezalishwa,”

Aidha, amesema wengi wao kati ya idadi hiyo yote ni vijana jambo ambalo linadhihirisha kwamba serikali ya awamu tano inatekeleza ipasavyo wajibu wake wa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini.

Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo kwa wawekezaji.

Prof. Ndalichako amebainisha kwamba kumekuwa na dosari ndogo ndogo katika maeneo ya kazi aliyoyatembelea ikiwemo baadhi ya waajiri kutotoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, kutowasilisha michango katika mifuko ya hifadhi kwa jamii pamoja na baadhi ya maeneo kutokuwa na mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.

Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri, amemshukuru Waziri Ndalichako kwa kufanya ziara katika Wilaya ya Kibaha na kuwakumbusha waajiri kuzingatia Sheria za Kazi ambapo ameahidi kushirikiana na wawekezaji katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amewataka wawekezaji kushirikiana kwa karibu na Ofisi yake katika kuboresha mazingira ya kazi.