Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ndalichako: Vijana Changamkieni Fursa ya Mafunzo Tarajali


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewataka vijana wanaohitimu kwenye vyuo mbalimbali nchini kuchangamkia fursa ya Mafunzo Tarajali yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi.

Waziri Ndalichako ameeleza hayo wakati wa ziara yake ya Kikazi alipotembelea Kitengo cha Huduma za Ajira (TAESA) hii leo Januari 25, 2022 Jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu kwa kukagua utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zilizopo chini ya Ofisi yake.

Akizungumza mara baada ya kuwasili katika ofisi hiyo amesema kuwa, Mafunzo ya Vitendo mahala pa Kazi “Internship Training” yamekuwa na tija kwa vijana wanaohitimu kwenye vyuo mbalimbali nchini kuweza kujengewa uzoefu na ujuzi wa kazi ili kumudu ushindani katika soko la ajira.

“Nimefurahi namna mafunzo haya Tarajari yanavyotekelezwa na kitengo hiki cha Huduma za Ajira, maana yameweza kuwajenga vijana kuwa na mtazamo chanya ambao umewasaidia waweze kujiamini katika misingi ya kazi,” alieleza Waziri Ndalichako

Aliongeza kuwa, kutokana na kazi nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa kuwa uhitaji wa mtu mwenye uzoefu, hivyo serikali iliamua kuja na mfumo huo wa mafunzo ya vitendo mahala pa kazi kwa lengo la kuwajengea vijana uzoefu na kukuza ujuzi wao.

“Serikali hii ni sikivu mno na ndio maana imeendelea kutengeneza mazingira wezeshi na kuongeza fursa za ajira kwa vijana kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa hapa nchini, Pia Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita serikali anayoiongoza imeendelea kuwa kivutio kwa wawekezaji ambao wamekuwa wakitoa fursa za ajira kwa wananchi” alisema

Aidha, Waziri Ndalichako alitumia fursa hiyo kuwasihi wawekezaji na pia waajiri katika sekta ya umma na binafsi kuendelea kutoa fursa kwa vijana wanaohitimu kwenye vyuo mbalimbali nchini ili waweze kuwa wazoefu na kujifunza kazi kwa vitendo katika maeneo ya kazi.

Pia, Mheshimiwa Ndalichako aliwataka vijana kuchangamkia fursa ya mafunzo hayo ya Utarajali yatakayowajengea uzoefu, maadili ya kufanya kazi, uzalendo na kuwafanya wawe wabunifu.

Sambamba na hayo, Waziri Ndalichako aliagiza Kitengo cha Huduma za Ajira kuhakikisha kinatoa mafunzo kwa vijana vyuoni ili kuwajengea ujasiri pindi wanapohitimu masomo yao waweze kupata utaalamu wa ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira.

Pamoja na hayo, amekiagiza Kitengo cha Huduma za ajira (TaESA,) kuwafuata vijana katika taasisi za elimu na kuwaeleza fursa za ajira na namna ya kukabiliana na soko la ajira hasa wale wanaokaribia kuhitimu masomo yao kwa kuwapa mafunzo maalumu ya kuwajengeaa kujiamini, namna ya kuandaa wasifu wao pamoja na namna ya kukabiliana na waajiri wao.

Kwa Upande Wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi ameendelea kuwasihi vijana kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kupitia mapato ya ndani, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Benki mbalimbali zilizopo nchini ili waweze kujiajiri na kuajiri wenzao.

“Serikali imeendelea kutoa fursa ya mikopo hiyo na kuweka mazingira wezeshi kwa kila mwananchi ili kuwawezesha waweze kutoa mchango wao katika kutengeneza wigo wa kujiajira pia,” alisema Katambi

Awali akizungumza Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira, Bw. Joseph Nganga alisema kuwa, Ofisi hiyo imeanzisha mfumo utakaowezesha vijana kupata taarifa ya fursa mbalimbali za ajira nchini na nje ya nchi, hivyo aliwataka vijana waliohitimu katika vyuo kujiunga na mfumo huo utawasaidia vijana wengi kuunganishwa na fursa za ajira.

Katika ziara hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alitembelea pia Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Kitengo cha Ukuzaji Tija (NIP) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA).