Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour and Employment Relations

News

Waziri Sangu ashiriki Hafla ya Taifa la Qatar


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Clement Deus Sangu ameshiriki katika hafla ya Siku ya Taifa la Qatar iliyoandaliwa na ubalozi wa Qatar nchini Tanzania.

Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 4 Desemba, 2025 katika hoteli ya Johari Rotana, Jijini Dar es Salaam ambapo Mhe. Clement Deus Sangu alikuwa Mgeni Rasmi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Clement Sangu amepongeza nchi ya Qatar kwa kuadhimisha siku hiyo ya taifa.

“Tanzania inatambua na kuthamini uhusiano wa kirafiki na wa kidiplomasia uliopo kati ya Qatar na Tanzania, tunaamini mshirikiano huu utaendelea kuimarisha sekta mbalimbali ikiwemo ajira, uwekezaji na fursa za maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Qatar,” amesema

Kwa upande mwengine, Mhe. Clement Sangu amesema kuwa Tanzania na Qatar zimeendelea kuwezesha nguvu kazi hususan vijana katika masuala ya ajira ambapo kwa mwaka 2025 kampuni ya usafiri ya Taifa la Qatar, MOWASALAT imetoa nafasi 800 za ajira mwezi Mei, Pia nafasi 1,092 za ajira mwezi Septemba kwa Watanzania katika nafasi ya madereva.

Naye, Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Mhe. Fahad Rashid Al Marekhi amesema, Qatar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali kwa lengo la kukuza maendeleo kati ya mataifa hayo mawili.

Katika hafla hiyo, Mheshimiwa Waziri Clement Sangu amekutana na kusalimiana na Mabalozi pamoja na viongozi mbalimbali.