Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Waziri Sangu: Serikali yaimarisha ulipaji wa Mafao na Pesheni


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe, Deus Sangu ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha mifuko ya Hifadhi ya Jamii inakuwa imara na inawahudumia vyema wanachama wake.

Mhe. Sangu ameyasema hayo Oktoba 12, 2026 mjini Sumbawanga wakati akifungua semina ya wastaafu zinazoratibiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Amesema tuna kila sababu ya kumpongeza Mhe. Rais wetu kwa kuhakikisha mifuko ya hifadhi ya jamii inaimarika ikiwemo na PSSSF.

“ Malipo ya mafao hivi sasa yanalipwa kwa wakati, serikali inaendelea kulipa madeni yake ya Mifuko ya hifadhi ya jamii, pensheni za mwezi kwa wastaafu zinalipwa kwa wakati na kuboresha kima cha chini cha pensheni kwa wastaafu, hakika hayo ni mafanikio makubwa ya awamu ya sita” alifafanua Mhe. Sangu.

Kadhalika amepongeza PSSSF kwa kuandaa semina hiyo na kueleza kuwa mafunzo hayo yatawaandaa wastaafu watarajiwa kwa ajili ya maisha sahihi baada ya kustaafu.

Kwa upande wa kauli mbiu ya PSSSF ya Tunalipa Jana, Mhe Sangu alisema, “Kulipa jana sio nadharia ni ukweli mtupu kwani wengi wamethibitisha, hakika shukrani tena ziende kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha PSSSF kulipa jana, hivyo kuweni na Amani kwani PSSSF ipo tayari kuwalipa”.

Akizungumza wakati akitoa salaam za mkoa, Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere aliishauri isitokee PSSSF ikawakwepa wastaafu watarajiwa wanapofatilia mafao yao, kwani ikitokea hivyo wastaafu watakata tamaa na kusononeka sana.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi akizungumzia utendaji wa Mfuko alisema, “Mheshimiwa mgeni rasmi hadi kufikia Juni 30, 2026 jumla ya wanachama 390,761 wameweza kulipwa mafao yenye jumla ya Shilingi Trillioni 12.94, na kwa sasa Mfuko una lipa mafao kwa wakati na una kauli mbiu yetu Tunalipa Jana.

Alisema, mafunzo yanalenga maeneo salama ya uwekezaji ambapo washiriki wataelimishwa umuhimu wa kuwekeza katika viwanda vidogovidogo na vya kati kwa kuzingatia uwezo wao, uwekezaji katika masoko ya fedha, kilimo biashara na ujasiriamali kwa ujumla. Katika kutekeleza azma hiyo washiriki watakutanishwa na taasisi salama za Fedha na uwekezaji kama ambavyo umewaona taasisi hizo wamekwishafika katika semina hii.

Semina hiyo inawezeshwa na wadau mbalimbali wakiwemo CRDB, NMB, NBC, AZANIA, AMANA, UTT, ABSA, ORBIT SECURITY na WHC. Wataalamu hawa wa fedha na uwekezaji, watawasaidia wastaafu watarajiwa wa Mfuko kuweza kubaini fursa za uwekezaji na jinsi ya kuwekeza vyema.