News
Wenye Ulemavu Wampa Tuzo Rais Samia
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, amepokea tuzo maalum kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutambua mchango wake mkubwa katika kuboresha Ustawi wa Watu wenye Ulemavu nchini.
Hafla ya utoaji wa tuzo hiyo imefanyika katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu iliyopo Oysterbay, Jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na taasisi ya Foundation for Disabilities Hope (FDM).
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Majaliwa amesema kuwa Rais Samia anaendelea kuthamini na kuunga mkono juhudi mbalimbali za kuwawezesha watu wenye ulemavu, na ameahidi kuendeleza jitihada hizo kwa vitendo.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuboresha sera, miundombinu na huduma zinazolenga kuhakikisha Watu wenye Ulemavu wanapata fursa sawa katika Elimu, Ajira na maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete pamoja na Naibu Katibu Mkuu Ofisi hiyoi walihudhuria hafla hiyo.