News
Wizara, Taasisi zapongezwa utekelezaji sera ya kinga ya jamii
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Mary Maganga, amepongeza wizara, taasisi na mashirika ya maendeleo ya kimataifa kwa ushiriki wao kwenye vikundi kazi vya utekelezaji wa sera hiyo, akisema kufanyika kwa kikao hicho kumedhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wadau wote wanashirikiana kuinua ustawi wa jamii.
Amesema ni wakati muafaka kwa wataalamu kushirikiana kuanzisha mfumo wa usajili (Social Registry) utakaosaidia kubainisha watu wanaohitaji huduma za kinga ya jamii na kuwezesha Serikali kufanya maamuzi sahihi.

Bi. Maganga alisema hayo , Novemba 27, 2026, wakati akifunga kikao kazi cha vikundi kazi wataalamu wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023 (Thematic Working Groups) mjini Morogoro.
Awali, Mkurugenzi wa Kinga ya Jamii toka Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi,Ajira na Mahusiano Festo Fute, alisema kikao hicho kimekutanisha vikundi kazi vinne ambavyo vimejadili na kukubaliana namna ya utekelezaji wa sera hiyo ili wananchi wengi wanufaike na huduma, ikiwemo misaada ya kijamii.
Vikundi hivyo ni Uzalishaji Jumuishi, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Uchangiaji, Misaada ya Kijamii na Huduma za Ustawi wa Jamii.
Fute aliongeza kusema jumla ya washiriki 60 kutoka wizara 11 na taasisi na mashirika 17 wameshiriki kikao hicho cha kwanza tangu vikundi hivyo kuanzishwa mwaka 2025.
Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni uelewa kuhusu kinga ya jamii himilivu (Adaptive Social Protection), utekelezaji wa sera ya taifa ya kinga ya jamii, mkakati wa ugharamiaji wa kinga ya jamii isiyo ya uchangiaji, pamoja na dhana ya kanzidata ya kusimamia afua za kinga ya jamii (Social Registry) na kanzidata ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF Registry).
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya washirika wa maendeleo, Jenifa Matafu kutoka UNICEF, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa jitihada za kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za kinga ya jamii.
Alisema wadau wa maendeleo, wakiwemo UNICEF na WFP, wataendelea kushirikiana kwa kuchangia rasilimali fedha na utaalamu na akatoa wito kwa Serikali kuboresha mfumo wa kisheria wa utoaji wa kinga ya jamii na kuhakikisha inajenga mfumo wa kanzidata ya kusimamia afua za kinga ya jamii, huku akieleza utayari wa WFP kutoa utaalamu kufanikisha azma hiyo.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Jabir Omar Makame, alisema Baraza litaendelea kusimamia sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ambayo wizara zote zinashiriki.
Alisema tayari NEEC, kwa kushirikiana na taasisi zinazotekeleza sera hiyo, zikiwemo NSSF, VETA na SIDO, inatekeleza mradi wa viwanda ambao umesaidia kuzalisha zaidi ya ajira 10,000 nchini.

