News
Wadau wa kazi na ajira watakiwa kushirikiana kutatua changamoto
Taasisi zinazohusika na masuala ya kazi na ajira nchini zimetakiwa kuimarisha ushirikiano katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya hifadhi ya jamii, ikiwemo masuala ya fidia kwa wafanyakazi wanaopata ajali, kuugua au kufariki kutokana na kazi zao.
Wito huo umetolewa Novemba 5, 2026, mkoani Morogoro, wakati wa uzinduzi wa Juzuu ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Compendium), iliyoandaliwa kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma za fidia na kuboresha utoaji wa huduma kwa wafanyakazi, sambamba na kuimarisha ushirikiano katika utendaji kazi kati ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mahakama ya Tanzania.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mheshimiwa Mustapher Siyani, alisema ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili na wadau wengine wa utatu, wakiwemo vyama vya waajiri, vyama vya wafanyakazi na wadau wa maendeleo, ni muhimu katika kuhakikisha haki za wafanyakazi zinalindwa na changamoto za sekta hiyo zinapatiwa ufumbuzi.
“Haki kazini haiwezi kujengwa na taasisi moja, bali kunahitaji Serikali inayoweza kusimamia sera na sheria, waajiri wanaotimiza wajibu wao, vyama vya wafanyakazi vinavyosimamia maslahi ya wanachama wao na taasisi za utoaji wa haki zinazofanya kazi kwa weledi, uhuru na ufanisi,” alisema Jaji Siyani.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, alisema ushirikiano kati ya WCF na Mahakama ya Tanzania katika kuandaa Juzuu hiyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu umuhimu wa taasisi za umma kushirikiana katika kuwahudumia wananchi na kutatua kero zao.
Alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha utawala wa sheria, kulinda haki na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi na utekelezaji wa masuala ya fidia kwa wafanyakazi nchini.
Waziri Sangu alieleza kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa katika usimamizi wa sekta ya hifadhi ya jamii, ikiwemo kuandaa Sera ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2023 inayolenga kupanua wigo wa ulinzi wa jamii nchini, pamoja na kufanya maboresho ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.
“Katika kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inalindwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeanzisha Fao la Utengamao (Rehabilitation Benefit) linalolenga, pamoja na mambo mengine, kuwapa ujuzi mbadala wafanyakazi wanaopata ulemavu kutokana na kazi ili waweze kuendelea kulitumikia taifa pamoja na hali zao ili kujipatia kipato. Maamuzi haya kwa kiwango kikubwa yameboresha mafao ya wafanyakazi na kuwapa uhakika wa kuendelea kupata kipato cha kukidhi mahitaji yao hata pale wanapopatwa na madhila yanayotokana na kazi” alisema Waziri Sangu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, alisema Juzuu hiyo ni matokeo ya ushirikiano wa kimkakati kati ya Mfuko huo na Mahakama Kuu ya Tanzania – Divisheni ya Kazi, wenye lengo la kuimarisha uelewa, tafsiri na utekelezaji wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.
Alisema katika kutekeleza azma hiyo, Mahakama Kuu ya Tanzania na WCF ziliandaa mafunzo maalumu kuhusu Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi yaliyowashirikisha Majaji 99 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, sawa na asilimia 95 ya majaji wote wa Mahakama hiyo kwa wakati huo, pamoja na Majaji 39 wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, ambao ni asilimia 100 ya majaji wa Mahakama hiyo.
“Natoa shukrani zangu za dhati kwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Jaji Kiongozi kwa ushirikiano wao katika kuidhinisha mafunzo hayo,” alisema Dkt. Mduma.
Uzinduzi wa Juzuu hiyo umeenda sambamba na Mkutano wa Kamati ya Utatu wenye kaulimbiu isemayo, “Kutoka Mazungumzo hadi Matokeo: Utekelezaji wa Majukumu ya Kamati ya Utatu kwa Maendeleo Endelevu ya Taifa.”
