Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Watumishi wa Umma muwe watumishi wa wananchi na muwatumikie kwa heshima - Rais Samia


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka watumishi wa umma kutumia mazingira bora ya kazi yaliyowekwa katika Mji wa Serikali Mtumba kuwahudumia wananchi kwa heshima, uadilifu, uwajibikaji na ufanisi.

Rais Samia ametoa rai hiyo leo, Oktoba 30, 2026, wakati akizindua majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami na miundombinu mingine muhimu katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Amesema Serikali imewekeza katika ujenzi wa majengo imara na ya kisasa pamoja na miundombinu inayowezesha watumishi kutekeleza majukumu yao katika mazingira bora, hivyo ni wajibu wao kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo chanya kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa pamoja na huduma mbalimbali kupatikana katika Mji wa Serikali Mtumba, wananchi hawapaswi kulazimika kusafiri hadi Makao Makuu ya nchi kufuatilia kila huduma ambayo inaweza kutolewa katika mikoa na wilaya wanazoishi.

Ameeleza kuwa Serikali inataka mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) itumike kikamilifu kuhakikisha huduma zinapatikana kwa urahisi katika maeneo ya wananchi, huku mifumo ya taasisi mbalimbali za Serikali ikiwasiliana na kubadilishana taarifa.

Ametoa mfano wa wananchi kutoka mikoa ya Rukwa, Kagera, Mtwara na Kigoma ambao hawapaswi kutumia muda na fedha nyingi kusafiri hadi Dodoma kufuatilia masuala yanayoweza kutatuliwa katika maeneo yao.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo ya TEHAMA ya Wizara na Taasisi za Serikali ili kuondoa urasimu na kuepusha wananchi kuhitajika kuwasilisha taarifa zilezile katika taasisi tofauti.

Rais Samia amesema teknolojia iliyowekwa katika Mji wa Serikali inapaswa kusaidia kurahisisha kazi, kuongeza tija na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amehitimisha kwa kuwataka watumishi wa umma kutambua kuwa dhamana waliyopewa ni kuwatumikia wananchi, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia misingi ya utumishi bora.